STORY;NDOA YANGU TRUE STORY MSIMULIZI:PILI MWANDISHI:BEKA - TopicsExpress



          

STORY;NDOA YANGU TRUE STORY MSIMULIZI:PILI MWANDISHI:BEKA MFAUME SEHEMU YA 13 Nilitamani nipige kelele ya kukanusha,lakini nilipoikumbuka mimba, nikanywea! Nani ningemtwisha mzigo huo? “Mimi nitafurahi umuoe binti yangu kabla hajajifungua,na unipe mahari ya shilingi laki tano! Unasemaje kwa hilo?” baba alisema. Sijui ni kwa nini ile hali ya juzi ya kupoteza fahamu kwa muda mfupi haikunitokea. Nilikuwa na dalili zote ambazo zingeweza kurahisisha tukio hilo litokee tena.Nilihisi kupoteza mawasiliano na mazungumzo hayo,ingawa nilizisikia sauti za watu wanaozungumza,lakini sikuelewa kilichokuwa kinazungumzwa. Nilikuwa sikufurahishwa na kauli ya baba! ************** Tokea kikao kile,nilianza kujiona kama goigoi. Maamuzi yote niliyoyapitisha awali kabla ya kikao kile kuanza,yakawa yamepotea. Kichwa changu kikawa kimeingia kiwingu cha sintofahamu iliyo mbele yangu,hata pale Victor aliponitaka turudi Pangani siku ileile mara baada ya kikao,nilijikuta nikimkubalia bila ya kuiingiza hoja niliyokuwa nimeiandaa ya kutaka nibaki hapo nyumbani angalau wiki moja. Tulirudi Pangani siku ileile. Jioni nilionana na Suzan na kumweleza kilichotokea Tanga. “Kwa hiyo wazazi wako wamekubali uolewe?” aliniuliza. “Wamekubali,” nilijibu. “Na wewe mwenyewe?” “Ningejibu nini?” nilisema nikishindwa kupata mwelekeo wa swali lake. Akaniangalia kwa macho yaliyokuwa yakiniambia, nakusikitikia Jacklin! “Kwa nini usingesubiri angalau mjijenge kwanza kimaisha?” aliniuliza. Nilikosa jibu la kumpa ingawa sikuiona dalili yoyote kama tungeweza kuyajenga hayo maisha anayokusudia Suzan. Aliniangalia mara moja baada ya kugundua nilikuwa sina jibu.Akaniaga na kurudi chumbani kwake.Kitendo kile cha kukatisha ghafla majadiliano na kuondoka kiliniumiza. Kulikuwa na mtazamo wa dharau kwenye macho yake aliponiangalia kwa mara ya mwisho.Ni wazi alikuwa akiniona siye yule Jacklin tuliyekutana kwa mara ya kwanza wakati tulipoingia chuoni,siye yule Jacklin aliyekuwa akipenda mambo ya kizungu, Jacklin mwenye hisia zilizokuwa zikiangalia maisha yake ya baadaye kwa mwelekeo wa mafanikio, Jacklin aliyekuwa akijigamba hafanyi kosa la kumchagua mwanamume asiye na uwezo… Nilishusha pumzi peke yangu, nikaiangalia hali ya mle chumbani ilivyo, iliyotawaliwa na samani chakavu na kukosa mvuto kwa kila kitu kilichomo mle. Hali ile ndiyo aliyoiona Suzan na wengine wote wanaokifahamu chumba hiki,chumba kisichomridhisha mtu yeyote atakayekiona,chumba ambacho kitawashangaza hata wazazi wangu endapo watakuja na kukiona na hawataamini kuwa nimekubali kuolewa ili niishi humo. Ilikuwa kama vile nikiwadhalilisha wazazi wangu! Sikuwa na jinsi,dalili zote zilinionyesha, hapa ndiyo patakuwa kwangu! Nilijiona kama mfungwa aliyehukumiwa kwenda jela kwa kosa ambalo hakukusudia kulifanya, akiingia kwa mara ya kwanza gerezani na kuonyeshwa chumba atakachoishi kwa muda wote wa kifungo chake! Sikujiona tofauti na mfungwa huyo! Usiku wa kwanza wa siku hiyo tuliyokuwa tumetoka Tanga, tukiwa kitandani,kwa mara ya kwanza nilimwona Victor akiwa amejilaza kimya huku akiwa anaangalia kwenye dari.Tulikuwa bado hatujazima taa,nilimwona akiwa hatikisiki zaidi ya kupepesa macho huku kichwa chake kikiwa kimeulalia mkono wake aliouegesha kisogoni.Sikujua alichokuwa akikiwaza,lakini nilikuwa na uhakika alikuwa akiyawaza yale yatokanayo na kikao kilichofanyika nyumbani. Sikumsemesha wala hakunisemesha,tukawa kimya kila mmoja akiwaza lake. “Jack!” aliniita. Nikageuka kumwangalia. Alikuwa haniangalii,bado aliendelea kuangalia juu. “Bee,” niliitikia kwa sauti ndogo. “Hivi nikikuoa sasa hivi, nitakupa nini cha maana hadi ujione kuwa umeolewa?” aliniuliza. Sikumjibu haraka.Nilikuwa nawazia jibu lipi sahihi la kumjibu.Kimya kilipita kati yetu,sote tukawa kama tunalifikiria swali lile kwa pamoja. Sikujua kwa nini aliniuliza vile.Nilitamani nimuulize,kwa nini alikubali angenioa,tena mapema baada ya kupewa hoja hiyo na baba.Nikahofia swali hilo lingeleta mtifuano usiku huo. “Kwani tangu unipe mimba hadi sasa tunaishije?” nilimuuliza. Hakunijibu! Aliinuka kutoka kitandani na kwenda kuizima taa kisha akarudi na kujilaza. Tukalala bila ya kusemeshana! ************** Tulianza rasmi maisha ya watu wanaosubiri kuoana. Kadri siku zilivyoenda ndivyo hali fulani ikawa inajitokeza kwetu.Hayakuwa maisha yale ya watu waliokuwa wakijiandaa kuoana,yetu yalikuwa tofauti.Tulikwenda kinyumenyume! Ukimya uliingia kwenye maisha yetu,kila siku mmoja wetu akawa anazidi kuwa mgeni kwa mwenzake.Muda wa kuwa pamoja nyumbani, tuliutumia muda huo bila ya kuwa na mazungumzo ya ukaribu huku kila mmoja akionekana kumkwepa mwenzake kadri ilivyowezekana na wakati mwingine tulikuwa tukipishana kiasi cha kugusana mabega bila ya mwingine kumsemesha mwenzake! Pamoja na kuwa hakukuwa na furaha kati yetu,lakini kukawa kumejitokeza kitu kimoja ambacho awali hakikuwepo.Kupigwa! Mambo yalikuwa yamebadilika,Victor hakuinua mkono wake kuthubutu kunipiga tokea tulivyorudi kutoka Tanga.Sikuwa na uhakika kama hilo lilitokana baada ya kugundua hali yetu ya maisha aliyoikuta Tanga haikuwa ya njaa-njaa,au ilitokana na mimba ambapo tumbo lilikuwa likiongezeka kila kukicha. Hakuwa mkali kwangu,hiyo nayo ikawa tabia mpya aliyoianzisha kwangu, pamoja na kutokuwa mkali lakini hakuwa na furaha. Hakunifurahia,lakini pia nilimwona kama vile hata yeye mwenyewe alikuwa hajifurahii. Alionekana kuumizwa na kitu kilichokuwa kinamtafuna ambacho hakuwa tayari kukiweka wazi kwangu! Kibaya zaidi,mwonekano wa kuwepo kwa dalili zozote za maandalizi ya kuolewa kabla sijajifungua,ulikuwa haupo, haupo kabisa! Haikunichanganya kwa sababu sikutaka kuolewa naye,lakini iliniweka kwenye njiapanda ya mustakabali wa maisha yangu! Baba alinipigia simu kama mara mbili kuniulizia kinachoendelea,nikamjibu kuwa,huwa simwelewi mwenzangu ana mpango gani,kwani hata kulizungumzia suala hilo halizungumzii! “Naomba umuulize ana mpango gani?” baba alisema. Nikamwitikia! Jioni Victor aliporudi kutoka kazini nikamwelezea jinsi baba alivyoniagizia nimuulize. “Nitakuoa bila ya kukulipia mahari?” aliniuliza. “Kwa nini jibu hilo usimwambie baba?”nilimuuliza. “Wewe si ndiye uliyepewa maagizo? Kwa nini asiniulize mwenyewe!” “Kwa hiyo, jibu hilo nimjibu baba?” nilimuuliza huku nikimwangalia.Alionekana kama hayuko sawa kichwani. Hakujibu! Baada ya siku kama nne kupita,baba alinipigia simu kutaka kujua kama niliongea na mwenzangu. Nikamweleza jibu nililopewa na Victor.Sijui kama jibu hilo naye lilimuudhi au vipi,lakini baada ya kumwambia hivyo, akanijibu kwa kifupi, “Basi nitazungumza naye!” Siku hiyo hiyo,mapema usiku nikiwa nimetoka kupiga soga chumbani kwa Suzan,nilirudi chumbani kwangu. Lakini kabla sijakifikia chumba changu,nikaiona pazia iliyopo mlangoni ikipepea kwa kujitumbukiza kwa ndani chumbani.Hali hiyo ikanijulisha kuwa mlango wa chumbani uko wazi ingawa nilipotoka nilikuwa nimeufunga kwa funguo.Nikahisi Victor amerudi kutoka matembezini. Nikiwa hatua chache kuingia chumbani,nikamsikia akizungumza kwenye simu. Nikataka kuingia hivyohivyo, lakini baada ya kubaini mazungumzo aliyokuwa akiyazungumza yakiniashiria kuwa alikuwa akizungumza na baba,nikasita kuingia. Nikasimama nje kumsikiliza, na sikutaka ajue kama nilikuwa eneo hilo nikimsikiliza. “Baba,mimi nakuomba uniruhusu nimuoe mwenzangu baada ya kujifungua,” alisema. “Hali yangu kiuchumi siyo nzuri hasa pia ukizingatia mwenzangu anatakiwa afanyiwe maandalizi maalum baada ya kujifungua…lakini baba…” Nikahisi kama aliyekatishwa. Kukawa kimya,nikajua baba atakuwa yupo kwenye kuzungumza.Baadaye nikamsikia Victor akisema, “Basi baba,kama umeamua hivyo,mimi nitamuoa kabla hajajifungua..!” Nilihisi maumivu yakikata tumboni,nikaondoka nilipokuwa nimesimama. Nikarudi upande uliko chumba cha Suzan,lakini kabla ya kuufikia mlango wake,nikageuza na kurudi nilikotoka.Nilikuwa nimechanganyikiwa na kauli ya Victor iliyoashiria alikuwa akilazimishwa na baba anioe kabla sijajifungua! Niliingiwa na maumivu ya moyo, nilimwona baba hanitendei haki kwa kutonitaka ushauri. Hili suala si la upande mmoja,hata mimi nilikuwa na haki ya kuulizwa kuhusu jambo hilo! niliwaza huku nikihisi kutokwa na machozi. Laiti ningeulizwa ningesema ndoa ifungwe baada ya kujifungua kwa sababu nilishakuwa na plani nyingine… Nilirudi taratibu kuelekea chumbani,nikajiondoa kwenye ile hali ya kulia kabla sijaingia.Nilimkuta Victor akiwa amemaliza kuongea na baba kwenye simu.Maungoni alikuwa na taulo alilojifunga kiunoni,nikatambua alikuwa amejiandaa kwenda kuoga. Tulisalimiana kwa salamu zenye ubaridi zisizo na bashasha na sikumuuliza chochote kuhusu nilichokisikia alichokuwa akikizungumza kwenye simu. Nilipoanza kumwandalia chakula,akatoka kwenda kuoga. Aliporudi alikikuta chakula nimekwisha mwandalia. Alikula kimya kimya,nadhani kama kuna alichonisemesha ni kuniuliza kama kuna pilipili. Baada ya kumletea aliendelea kula.Mimi nikawasha runinga na kuwa mwenza wangu. Hakuna aliyemsemesha mwenzake hadi alipomaliza kula. Niliinuka na kuviondoa vyombo alivyokulia huku nikiacha gudulia lenye maji na glasi.Niliviingiza vyombo vilivyotumika kwenye sufuria kubwa iliyomo humo chumbani na kufunika kwa juu sufuria nyingine kwa kuhofia panya wadogo waliokuwa sehemu ya familia yetu. Kisha nilirudi na kuendelea kuangalia runinga.Akiwa bado hajaondoka alipokuwepo,nilimwona akijimiminia maji yasiyokuwa baridi kutokana na kutokuwa na jokofu na kutia kwenye glasi. Sikumwangalia alivyokuwa akinywa,lakini sehemu ya macho yangu yalimwona alivyokuwa akinywa. Alikunywa kwa mkupuo bila ya kuondoa glasi kinywani hadi alipomaliza na kuishusha glasi mezani ambayo ilitoa sauti ya mgoto wake.Kisha akafanya kitu kilichokuwa kikiniteketeza siku hadi siku.Alipiga mbwewe iliyotoa sauti ya kujivuta huku mwenyewe akionekana kuifurahia. Niliacha kuangalia runinga na kumwangalia kwa jicho la hasira.Nadhani alikuwa akijua kuwa nilikuwa nikimwangalia.Ghafla alinitupia jicho na kuniona namwangalia,hakunijali! Ndiyo kwanza alianza kusafisha koo lake kwa kufanya mkwaruzo uliotokea kooni na kulizaliza mdomo wake kutokana na kuondoa mabaki ya chakula kwa kutumia ulimi wake.Ilikuwa kama vile alikuwa akinifanyia kusudi! Nilikuwa nimeshamchoka, chuki dhidi yake ikawa maradufu! Hadi tunakwenda kulala, hakunigusia lolote kuhusu simu aliyopigiwa na baba! Wiki ikapita bila ya kuniambia lolote kuhusu mazungumzo hayo! ITAENDELEA KESHO MUDA KAMA HUU USIPITE BILA KU-LIKE NA KU-COMMENT ILI TUJUE WANGAPI TUPO PAMOJA
Posted on: Sat, 14 Sep 2013 17:26:33 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015