Mahakama ya Madawa ya Kulevya Itawahukumu Mapapa na Manyangumi au - TopicsExpress



          

Mahakama ya Madawa ya Kulevya Itawahukumu Mapapa na Manyangumi au Itaendelea na Vidagaa..!! Hivi karibuni waziri mkuu Mizengo Pinda amekaririwa akisema kwamba Serikali ina mpango wa kuanzisha mahakama maalum ya kushughulikia kesi za madawa ya kulevya. Kauli hii ya Serikali imekuja baada ya vyombo vya habari kuiweka wazi mitandao ya madawa ya kulevya hapa nchini, hata hivyo pamoja Serikali hii ya awamu ya nne kukubali na kuzungumzia tatizo la nchi kukumbwa na janga la madawa ya kulevya, lakini biashara ya madawa haya ya kulevya imeanza miaka mingi. Madawa ya kulevya ndicho kipimo cha kwanza kinachotumika na jumuiya za kimataifa kutathimini uhalali wa Serikali yoyote iliyopo kwenye madaraka katika nchi husika; ukikuta nchi imekumbwa na janga la madawa ya kulevya hiyo inadhihirisha wazi kwamba kwenye nchi hiyo hakuna Serikali ya wananchi, bali kuna Serikali ya watawala na vyombo vyake vya ulinzi na usalama ambavyo huwa kazi yao kubwa ni kulinda Serikali hiyo ya watawala inayokumbatia biashara ya madawa ya kulevya! Pia Serikali ya watawala hakuna sheria, na kama hakuna sheria ina maana kwamba hakuna haki hasa kwa wananchi wa kawaida! Madawa ya kulevya ni kipimo cha kwanza cha kiwango cha uhalifu na uvunjikwaji wa sheria katika jamii husika; madawa ya kulevya ndicho kipimo halisi cha kupima kiwango cha mauwaji ya kupangwa; madawa ya kulevya ndiyo njia sahihi ya kupima kiwango cha maambukizi na waathirika wa ugonjwa wa ukimwi katika nchi husika; madawa ya kulevya ndiyo kishawishi kikubwa cha kuingiza nchini silaha haramu na matumizi mabaya ya silaha hizo kinyume cha sheria; madawa ya kulevya ni chanzo cha kuwa na matajiri wengi nchini wenye pesa za kutisha lakini hawalipi kodi! Uwezo wa kununua ni mkubwa sana kwa watu wachache wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya! Kulingana na ripoti iliyotolewa hivi karibuni na World Bank na IMF Tanzania imeonyeshwa kwamba ina uchumi mzuri ukilinganisha na nchi nyingi za Kiafrika na hata kidunia; kwa mfano Tanzania imetajwa kuwa ni nchi ya 85 duniani kwa kuwa na kiasi kikubwa cha PPP (Purchasing Power Parity) yaani uwezo wa sarafu wa kununua bidhaa ya aina ile ile kwenye nchi mbili tofauti kwa wakati ule ule. Taarifa hizi pamoja kwamba zimetolewa na taasisi za kimataifa lakini mimi nazipinga kwamba siyo sahihi! Kiwango hicho cha PPP siyo kwa ajili ya Watanzania bali ni kwa wale wote wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya wakishirikiana na watawala wetu ambao hasa ndiyo wanaohakikisha kwamba unga unaingia kiusalama na kusafirishwa kwenda kuuzwa nchi za nje kiusalama bila ya bughudha zozote! Ukitaka kilithibitisha hili kiurahisi nenda kwenye soko la magari, ma-super market makubwa na soko la viwanja, mashamba na nyumba; utakuta kwamba wengi wanaonunua bidhaa hizi kwa mkupuo ni wale wanaojihusisha biashara za madawa ya kulevya. Kwa mfano, bei ya kununua kiwanja maeneo ya Oysterbay, Masaki na Mikocheni jijini Dar es Salaam ni ghali mara mbili kuliko bei ya kiwanja cha ukubwa huo huo katika majiji ya Johannesburg, Cape Town, Durban au Cairo hii ni miji mikubwa na tajiri katika bara la Afrika! Hivi ndivyo wachumi wanavyotathimini uwezo wa sarafu moja kununua bidhaa kwenye nchi mbili tofauti kwa wakati ule ule, au kwa jina la kigeni “Purchasing Power Parity (PPP)” ninachotaka kusema ni kwamba PPP yetu ipo juu, lakini haipo juu kwa kwamba uchumi wetu ni mkubwa, hapana, ipo juu kwa vile kuna watu wachache wanaomiliki pesa chafu zinazotokana na biashara ya madawa ya kulevya, na hawa hasa ndiyo wamesababisha mfumuko wa bei kwenye bidhaa kama magari, majiko ya kupikia, friji, Laptop, Simu za mikononi, mashine za kufulia, viyoyozi, na Real Property (Mashamba, viwanja na nyumba); hizi ni baadhi ya bidhaa ambazo hutumiwa na wachumi wa kimataifa katika kupima uwezo wa kununua wa jamii moja hadi nyingine. Watu wachache wenye pesa haramu zisizolipiwa kodi wamezifanya baadhi ya bidhaa muhimu kupanda bei na kununuliwa kwa viwango vile vili zinazonunuliwa na walaji wa nchi matajiri! Hii kiuchumi wanaiita “Demand Pull Inflation” Wazungu wa Unga wanauponza umma wa watanzania uonekane una Madola mengi ya Kimarekani mifukoni mwao kumbe wengi wetu hata bei ya sukari hatujui ni shilingi ngapi!? Kabla sijarudi kwenye Mahakama ya Madawa ya Kulevya kwanza nataka niangalie ni akina nani hasa hapa nchini wanaojihusisha na biashara hii ya madawa ya kulevya? Nikilijibu swali hili pia nitaelezea hali halisi ya soko la madawa ya kulevya hapa nchini na masoko mengine ya nchi za nje. Wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya hapa nchini ni viongozi wa Serikali wa ngazi za juu wakishirikiana na wafanyibiashara wakubwa hapa nchini, pamoja na wabunge, wanasiasa, viongozi wa makanisa mbalimbali hapa nchini, wote hawa wakiwezeshwa kwa kushirikiana na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, hasa kitengo cha usalama wa taifa (TISS) na jeshi la polisi nchini! Huo ndiyo mtandao wa wadau wakubwa wa biashara ya madawa ya kulevya hapa nchini. Na kuthibitisha maneno yangu haya hivi karibuni waziri katika ofisi ya rais William Lukuvi alikiri kwamba wabunge ndiyo vinara wanaoshutumiwa kwa kujihusisha na biashara ya kulevya! Kwani wabunge ni akina nani? Wabunge si ndiyo viongozi wa umma wanaotunga sheria bungeni, wao ndiyo mawaziri, wao ndiyo mabalozi, wao ndiyo makatibu wakuu wa wizara, na wao ndiyo viongozi wakuu wa Serikali! Kulingana na ukweli huo kwamba wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya ni viongozi wa ngazi za juu wa Serikali na umma kwa ujumla, na viongozi hawa wasingelifanikiwa kufanya biashara hiyo peke yao kama wangelikuwa siyo washirika wakuu wa TISS na jeshi la polisi! Kwa mfano, kama inatokea kwamba rais anajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya; makamu wa rais anajihusisha na madawa ya kulevya; waziri mkuu anajihusisha na madawa ya kulevya; baraza la mawaziri linajihusisha na madawa ya kulevya; wabunge wote wanajihusisha na madawa ya kulevya; marais wastaafu; mawaziri wakuu wastaafu na mawaziri wastaafu wote wanajihusisha na madawa ya kulevya; viongozi wote wa kidini wanajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya; matajiri wakubwa wote nchini wanajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya; majenerali wote wa JWTZ wanajishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya; wakurugenzi wote na maafisa wa ngazi za juu wa TISS wanajishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya; mahakimu na majaji wote wanajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya; maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la polisi wanajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya! Je, katika mazingira kama haya wananchi wanaweza kushinda vita dhidi ya madawa ya kulevya!? Soko la madawa ya kulevya hapa nchini siyo kubwa sana na walaji wa madaya hayo ni vijana wadogo ambao wamekuwa wahanga wa jaribio la kuboresha soko la wala unga hapa nchini; watanzania walizoea kuvuta Bangi ambayo hulimwa sehemu mbalimbali hapa nchini. Madawa ya kulevya kama vile Cocaine, Heroine, Mandrax na mengine, hizi ni bidhaa toka nje ya nchi hasa hulimwa katika nchi za Columbia, Afghanistan, Pakistan, Uzbekistan, Tajikistan, Kyrgyzstan, na nyinginezo. Vijana wa Kitanzania waliokumbwa na janga la kujiingiza kwenye madawa ya kulevya wamegawanyika makundi makubwa mawili: kundi la kwanza ni lile linalohusishwa na maslahi ya kisiasa kwa vile wanasiasa wana mbinu nyingi za kulinda nafasi zao zisije kuchukuliwa na wale wengine walioko nje ya mduara wa kula, hivyo basi vijana wala unga wameweza kulinda mashahi ya kisiasa; na kundi la pili ni lile ambalo vijana wamejiingiza kwenye tamaa ya kutaka kuishi maisha ya kifahari, na kujikuta wanabebeshwa unga kwa ahadi kwamba wakifikisha mzigo salama huko unakokusudiwa, basi wataachana na kupanda dala dala na kuendesha Mercedes Benz au BMW nakadhalika! Kundi la kwanza la kisiasa limeathiri vijana wengi wa kawaida ambao wamejikuta kujiingiza katika utumiaji wa madawa ya kulevya bila ya kuwa na malengo yoyote! Wengi wao ni vijana wa shule za sekondari wameiga tu kwa vile amewaona wenzake wanatumia, bila ya kutafakari faida na adhari za madawa hayo. Bangi nyingi inayolimwa hapa nchini husafirishwa nchi za nje, na masoko makubwa ya Bangi ya Tanzania kwa nchi za Kiafrika ni South Africa, Visiwa vya Seychelles, Visiwa vya Maurtius, Visiwa vya Comoro, na Visiwa vya Reunion. Hizi ndizo nchi wanunuzi wakubwa wa Bangi ya Tanzania, na Bangi hii husafirishwa kwa mitumbwi inayoondokea njia za panya na nyingine hupitia bandarini na husafirishwa kwa meli, wakati mwingine hata ndege hutumika kusafirisha Bangi ya Tanzania. Kuhusu madawa ya kulevya kama vile Cocaine na Heroine ambayo hayalimwi hapa nchini, ni kwamba kwa vile wanaojihusisha na biashara hii ni aidha viongozi wa Serikali au watu wenye ushawishi mkubwa serikalini, hivyo basi wameweza kutumia mamlaka yao na ushawishi wao kwa kusimamia uingizwaji wa madawa hayo hapa nchini na kuyasambaza kwenye zile nchi ambazo wana wateja wakubwa wa madawa haya; njia za kuyasambaza madawa haya zipo nyingi zikiwemo meli au ndege, na wanaotumiwa kubeba madawa haya ni vijana wa Kitanzania ambao wamefundishwa namna kumeza madawa hayo au kuyaficha sehemu za siri ambazo si rahisi kuonekana! Wanunuzi wakubwa wa madawa ya kulevya ya kutoka Tanzania wapo South Africa, nchi za Asia, nchi za Uarabuni na nchi za Ulaya. Jeshi la polisi pamoja na wafanyikazi wa kitengo cha usalama wa taifa ni lazima wawe wanajua kwamba ni akina nani wanaoingiza na kutoa madawa ya kulevya hapa nchini. Rais Kikwete amewahi kupewa mara mbili orodha za mapapa na manyangumi wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya hapa nchini, na katika orodha hizo walikuwepo mawaziri, wabunge, viongozi wa ngazi za juu wa Serikali, wanasiasa, wafanyibiashara maarufu hapa nchini na maaskofu wa makanisa mbalimbali hapa nchini! Inasemekana kwamba kuna Askofu mmoja hapa nchini jina lake linahifadhiwa waumini wasije wakajalisusia kanisa; Askofu huyo alipoulizwa kwanini wewe ni Askofu halafu unajihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya!? Alijitetea kwa kusema “Mheshiwa, nisamehe, ni kweli najihusisha na biashara hiyo haramu ila sipo peke yangu, bali nashirikiana na wabunge wako wanne” Alipowataja wabunge hao ambao si wabunge tu bali pia wana nyadhifa kubwa za kitaifa!! Mheshimiwa akaishiwa nguvu kabisa, ilibakia kidogo apate ugonjwa wa moyo..!! Vita dhidi ya madawa ya kulevya ikaishia hapo..!! Kuna nchi moja ambayo sitaki kuitaja jina, lakini nchi hii wananchi wake walishawahi kuandamana wakiunga mkono kutoa na kupokea rushwa; nchi hiyo kiwango cha Rushwa katika idara mbalimbali za Serikali na jamii kwa ujumla kinakadiriwa na kuingizwa kwenye pato la taifa (GDP) kila mwaka! Hivyo na sisi tukiendelea na kasi hii hii ya madawa ya kulevya itafikia mahali tutaona hakuna budi ya kuingiza mapato yanayotokana na biashara ya madawa ya kulevya kwenye pato letu la taifa (GDP) kila mwaka! Hata hivyo inaonekana makadirio ya World Bank na IMF kuhusu pato la taifa la Tanzania siyo sahihi, kwa vile mabilioni ya dola za Kimarekani ambazo ni pesa chafu inayotokana na madawa ya kulevya na haiingizwi kwenye pato la taifa; nasema ni mabilioni kwa vile biashara hiyo hapa nchini ina mtandao mkubwa na ulioendelea hasa ukizingatia kwamba una mkono wa Serikali. Sasa narudi kwenye mpango wa Serikali wa kutaka kuanzisha mahakama maalumu ya kusikiliza kesi za madawa ya kulevya; tumeona kwamba wanaojihusisha na biashara hii ni viongozi mbalimbali wa Serikali na umma wakishirikiana na wafanyibishara mashuhuri na viongozi wa kidini! Na hii ndiyo sababu inayosababisha kesi za madawa ya kulevya kutokufikishwa mahakamani; na hata zile zilizofikishwa mahakamani aidha hazikusikilizwa au zilifutwa au zimekuwa zikiendelea kupigwa kalenda! Kwanini tuanzishe mahakama mpya wakati hizi zilizopo zimeshindwa kuwashughulikia wahalifu wa bishara ya madawa ya kulevya, licha ya kwamba ushahidi na vithibitisho vyote vipo wazi! Je, tunajenga majengo mapya peke yake, au pia tutawafundisha mahakimu na majaji wapya kozi maalumu ya kushughulikia kesi hizi za madawa ya kulevya, au ni wale wale wa zamani ndani ya majengo mapya!? Je, tutapata wapi waendesha mashtaka wapya, au tutawachukuwa hawa hawa walioshindwa kazi kwa kuendekeza ufisadi!? Sawa tutaanzisha mahakama maalumu, lakini tutawapata wapi mahakimu na waendesha mashitaka wapya wasiokuwa na hulka za rushwa!? Labda tuombe waendesha mashitaka, mahakimu na majaji wa kutoka European Union waje waziendeshe mahakama zetu za madawa ya kulevya! Tumegundua kwamba tatizo la kesi za wauza unga kutokushughulikiwa siyo uchache wa mahakama, hapana, bali tatizo ni viongozi mbalimbali wa Serikali na wale wa umma wakishirikiana na wafanyibishara wakubwa na viongozi wa kidini ndiyo vinara wa biashara hii, na hawa ndiyo wenye mamlaka na ushawishi mkubwa kwenye vyombo vyote vinavyosimamia sheria nchini kama vile: Jeshi la Polisi; Kitengo cha Usalama wa Taifa (TISS); Takukuru; Waendesha Mashtaka; Mahakimu na Majaji. Hawa wote kulingana na utaratibu ambao tumeamua kuingoza nchi yetu wamejikuta wakiwa na uhusiano wa karibu au wadau wa wafanyibiashara ya madawa ya kulevya kwa sababu mbalimbali, na hivyo kuwafanya washindwe kutenda haki kwa kuwatetea na kuwalinda wauza unga! Tumegundua kwamba kuanzisha mahakama maalumu ya kusikiliza kesi za madawa ya kulevya siyo suluhu ya matatizo yetu ya kupambana na biashara ya madawa ya kulevya; mimi naona mahakama maalumu zikianzishwa zitaendeleza hulka za vitendo vya ufisadi hapa nchini na kuwafanya waendesha mashitaka, mahakimu na majaji wa mahakama hizo kuendelea kuchukuwa rushwa; tena mimi naona mahakama hizo zikianzishwa zitapandisha kiwango cha rushwa na kuwa kikubwa zaidi kuliko hiki wanachotoa sasa hivi! Ina maana kwamba kuanzishwa kwa mahakama hizo maalumu kutawaneemesha kwa rushwa zaidi wafanyikazi wote wa idara na vyombo vya kusimamia sheria kama vile: Jeshi la Polisi; Kitengo cha Usalama wa Taifa (TISS); Takukuru; Waendesha Mashtaka; Mahakimu na Majaji. Tunaweza kuanzisha mahakama maalumu ili kuwafariji walipa kodi waone Serikali yao inajitahidi kupambana na wahalifu wa biashara ya madawa ya kulevya, ila kuikweli hakuna matokeo mazuri ya hilo zaidi ya kufuja kodi za wananchi zitakazotumika kuziendesha mahakama hizo! Tatizo letu kubwa hapa nchini ni kukumbatia utawala wa matabaka: tabaka la watawala ambalo linaundwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wa ngazi za juu na wafanyibiashara maarufu nchini; na tabaka lingine ni lile la watawaliwa ambalo linaundwa na watu masikini na wananchi wa kawaida wa mijini na kule vijijini. Tabaka la watawala lipo juu ya sheria, kesi zao hazifikishwi mahakamani bali huzungumziwa huko Ikulu, na hata ikatokea bahati mbaya ikafika mahakamani, lakini itapigwa dana dana na mwisho hukumu yake itakuwa hailingani kabisa na kosa lililotendeka! Isipokuwa mtuhumiwa anayetoka kwenye tabaka la watawaliwa kesi ndogo anapewa adhabu kubwa na hukumu hutolewa mara moja bila usumbufu! Hii inaonyesha kwamba sheria, mahakama na magereza ya Tanzania vipo kwa ajili ya tabaka la watawaliwa na ndiyo maana mahakama zetu zimeshindwa kutenda haki kwenye janga la bishara za madawa ya kulevya kwa vile wadau wakubwa wa biashara hii ni wale wanaotoka kwenye tabaka lililopo juu ya sheria ambalo ni tabaka la Watawala, na ndiyo maana kwenye kichwa cha makala yangu nimesema “Mahakama ya Madawa ya Kulevya Itawahukumu Mapapa na Manyangumi au Itaendelea na Vidagaa..!!” noordinjella.livejournal
Posted on: Fri, 13 Sep 2013 16:00:15 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015