RIWAYA: MTAFITI MTUNZI: HUSSEIN TUWA SEHEMU YA MWISHO -PART - TopicsExpress          

RIWAYA: MTAFITI MTUNZI: HUSSEIN TUWA SEHEMU YA MWISHO -PART 3 “Seriously?” Mrakibu aliuliza, na hapohapo akaongezea, “Namtaka Luis Kambesera sasa hivi! Nitamhojimimi mwenyewe bloody shenzi! Atasema ni nini kinaendelea kati yake na huyu mbunge shenz Taipp! Namtaka!”Mrakibu alifoka. “With pleasure sir!Hivi niko njiani kwenda kumtia nguvuni…wenzake wote wako mikononi mwetu tayari. Taarifa nilizo nazo ni kwamba bado yuko ofisini kwake…” Kwakwa alimjibu huku akiendesha gari la polisi kuelekea Liquid Diamond, Sajenti Pojo akiwa kando yake mle garini… _______________ Luis Kambesera aliteremka kutoka kwenye lifti na kuingia kwenye ukumbi wa pale mapokezi kwenye ghorofa ya chini kabisa ya lile jengo lenye ofisi za kampuni yao, Bilanga akiwa nyuma yake. Walishangaa kidogo kuona ule ukumbi ukiwa kiza, lakini hawakujali, kwani walikuwa wanaondoka kimoja. AIikuwa ameshapiga simu kwenye kampuni ya ndege ya kukodi ambayo ilikuwa ikimsbiri uwanjawa ndege tayari kumtoa nje ya nchi usiku ule ule. Mkononi alikuwa ameshika mkoba wa safari ambao ndani yake kulikuwa kuna rundo la hela na cheki za kusafiria, naBilanga naye alikuwana begi jingine lenye hela pia. “Mnasafiri usiku-usiku Luis?” Sauti ya Inspekta Kwakwa iliwafikia palewalipokuwa kutokeakwenye kona moja ya ukumbi ule,na wote wawili wakahamanika. Bilanga alitoa bastola na kuielekza huku na huko mle ndani bila kumuona msemaji. “Jitokeze wewe!Jitokeze!” Alibwata kwa hasira. Lakini kote kukawa kimya. Luis alitoka mbio kuliendea lango la kutokea nje ya jengo lile na kujikuta akikwama pale mlangoni, ule mlango ukiwa umekomewa kwa nje. “Hah!What the…?”Aliusukasuka kwanguvu ule mlango huku akiwa amehamanika vibaya sana, na wakatihuo huo Bilanga akielewa kuwa polisi walikuwa wamewanasa, alianza kurudi nyuma taratibu huku akiilengesha bastola yake huku nahuko, tayari kumshambulia yeyote atakayejitokeza mbele yake. Ghafla mwanga mkali sana wa kurunzi kubwaukammulika usoni kutokea mbele yake. “YAAAAARGHH!” Bilanga alipiga ukelele na hapo hapao akafyatua risasi, na akashtukia akipigwa teke kali mkononi na ile bastola yake ikatupwa pembeni. “HAH!” Taa zikwaka ghafla mle ndani, na Luis akabaki akiwa amejiegemeza mlangoni huku ametumbua macho, akishuhudia askari watatu wenye silaha, wawili wakiwa wamemuelekezea yeye zile silaha zao, mmoja akiwa amemuelekezea Bilanga, ilhali Inspekta Kwakwa akiwa amemsimamia Bilanga mbele yake bila silaha yoyote. Duh! “Mmeingiaje humu nyinyi?” Luis alimaka kwa woga. Kwakwa alikuwa anatazamana naBilanga kwa hasira. Bilanga alibaki akitweta kwaghadhabu huku amejishika mkono wake uliopanguswa kwa teke la Kwakwa. Bila ya kuondoa macho yake kwa Bilanga, Kwakwa alimwambia Pojo. “Huya fala akikwepua tu piga risasi ya goti, sawa?” “Yes Sir!” Pojo alijibu huku akiikoki bastola yake na kuzidi kumuelekezea Bilanga. Kwakwa akamuendea Luis, na kumtazama kwa macho yaliyojaa dharau. “Unakumbuka kuwa nilikwambia kwamba akili nyingi hupoteza maarifa Luis?”ALimuuliza. “Toka hapa!Huna lolote la kunikamatia mimi! Huna ushahidi!” Luis alimaka, na Kwakwa akamcheka. “Nimeiona ripoti ya Grayson Mochiwa Luis…ile ambayo wewe uliificha na ukatoa ya kwako uliyoichakachua…ukishirikiana na swahiba wako kutoka bungeni!” Almwambia na Luis alitumbua macho kwa kutoamini. “Nahitaji wakili wangu!” Alibwata, na Kwakwa akamcheka tena. “Uko chini ya ulinzi Luis Kambesera…wakili wako atakukuta huko huko mahabusu, shwaini tasa we!” Kwakwa alimkemea kwa hasira, kisha akamgeukia yule askari wa kike aliyetoka kwenye kitengo cha John Vata.“Piga pingu huyu!”Alibwata. Luis aliangua kilio huku akipigwa pingu. Kwakwa akamrudia Bilanga huku akitoa pingu yake. “Wewe nakutia pingu mwenyewe, kichwa ka’ kokwa ya mbirimbi!”Alimwabia huku akimning’inizia pingu usoni. “Kwa kosa gani?”Bilanga alijitia kuweka kibesi. “Kwa mauaji ya Mwamtumu Uledi! Na kushiriki katika njama za kumuua Grayson Mochiwa, na kushiriki katika njama za kulihumu taifa…oh, Bilanga mlolongo ni mrefu sana! Leta kono hilo nilitie pingu wewe!”Kwakwa alimwambia kibabe. “Unapata jeuri kwa kuwa uko na wafuasi wako wenye silaha hapa, sio?”Bilanga alimtemea maneno ya hasira. “Hata ningekuwapeke yangu nabila silaha… mi nakutia nguvuni tu Bilanga…sio ligi yako mimi wewe!” Kwakwa alimjibu huku akimshika mkono ili amfunge pingu, lakini Bilanga akachomoa mkono wake kwa hasira. “Niache! Kama ungekuwa peke yako we’ usingetoka mzima leo hii, pusi mkubwa!” Bilanga akamwambia. Kwakwa akamtazama kwa hasira. “Okay…Pojo na wote nyie! Shusheni silaha zenu chini…naasiingilie yeyote hapa. Nataka nimpe nafasi kichwa thumni hapa kunionyesha ubabe wake!”Alisema huku akitandaza mikono yake tayari kupambana. “Hah! Afande! Una hakika…?” Mmoja wa wale askari wa Vata alimaka na Pojo akainglia kati. “Si mmemsikia alivyosema?Wote shusha silaha, kaeni pembeni!” Alisema huku akishusha bastola yake na akirudi nyuma. Bilanga hakuuweka. Aliunguruma kwa hasira na kumrukia Kwakwa kwa bichwa la nguvu lililojikita katikati ya kifua na tumbo lake, na kumkumba hadi chini. Kwakwaaliachia ukelele wa mshituko na pumzi ikamtoka wakati akienda chini, Bilanga akiwa juu yake. Hapo hapo Kwakwa alitumia mtindo wa judo na kumtupa hewani yule jamaa kwa miguu yake, naye akajibingirisha pembeni wakati Bilanga akiangukia mgongo kwa kishindo pale sakafuni. Bilanga aliuguruma tena huku akijiinua haraka na kugeukia kule alipojua kuwa Kwakwa alikuwako, akakutana na teke zito la upande wa kulia wa uso wake naye akayumba kushoto.Akgeuka kwa hasira kule lilipotokea lile teke. Kumbe Kwakwa hakuwa ameushusha ule mguu wake uliomtandika lileteke la kwanza, akamtandika tele la pili kwa mguu uleule upande wa kushoto wa uso wake na Bilanga akapepesukia kulia. Kwakwa akaushusha mguu wake haraka, akaudundisha chini kisha akaenda hewani huku akiukunjua mguu wake mwiginena kumfyatua teke jingine kali la kidevu. Bilanga akatupwa nyuma kama gogo, wale askari wakianchia miguno ya mshangao. Bilanga alisambaratika sakafuni nakujiinua haraka, damu ikimvuja kinywani, lakini akaenda tena chini bila kupenda. Kwakwa alibaki akiwa anaruka ruka kimakabiliano, akimtazama kwa makini. Bilanga alimtazama kwa hasira na katema rundo la mate mekundu sakafuni. Akainuka na kumuedea mbio kwa hasira, akiwa amekunja ngumi, na kwa hatua isiyotarajiwa Kwakwa aliruka hatua moja mbele na kwenda hewani na kumshndilia miguu yake yote miwili kifuani. Bilanga akatuptwa tena nyuma huku akiachia mgunowa maumivu na kujipigiza ukutani kwa kishindo, kabla ya kusambaratika sakafuni kama gunia tupu. Akabaki akitweta pale chini. Kwakwa akamfuata na kumzunguka pale alipokuwa. “Ulikuja kutushambulia kwa bomu la machozi sisi paka wewe, eenh?” Alimuuliza kwa hasira, na kumtandika teke kali la kichwa, na jamaa akagaragazwa sakafuni kwa msukumo wa teke lile, akigumia kwa uchungu. Akajitahidi kuinuka, na kufanikiwakupiga goti moja pale chini, akitikisa kichwakuweka akili sawa. “Halafu ukajitia kuja kumtorosha Chabbi akiwa mikononi mwetu?”Alimuuliza na kumtandika teke jingine la uso, na jamaa akatupwa nyuma kwa nguvu, damu nameno vikiruka kutoka kinywani mwake, yule askari wa kike akiachia kilo cha woga. Bilanga akajibwaga chali pale chini, akiwa ametwanya mikono yake huku na huko, ilhali miguu ikiwaimemtawanyika vile vile, damu ikimvuja kinywani na akitweta kwa taabu. Luis hakuamini macho yake. “Piga pingu mzoga huu tuondoke nao, bloody shit!” Kwakwa alisema kwa hasira huku akijikung’uta mikono yake. “Duh!Si mchezo aisee!” Yule askari wa Vata alisema wakati Pojo akimgeuza Bilanga kifudifudi na kumfunga pingu kwa nyuma. Luis na kibaraka wake walitolewa nje ya jengo lile wakiwa chini ya ulinzi, ihali Blanga akiwa hana fahamu. Wale walinzi wa ile kampuni binafsi ya ulinzi walibaki wakikodoa macho bila ya kuaminini kile kilichokuwa kimetokea usiku ule. _______________ “Msweke ndani mpaka kesho asubuhi, aonje raha ya lupango kwanza. Nitakuja kumhoji mwenyewe!” Mrakibu alisema alipopewa habari kuwa tayari Luis yuko mbaroni. Usiku ule ule Kwakwa na Pojo waliandaa ushahidi wao dhidi ya wale watuhumiwa waliowakamata, wakiandika ripoti kamili ya kila kilichojiri. Kwakwa akampigia simu Inspekta Kelvin. “Inspekta, naona umuachie tu huyo mganga wa kienyeji…wauaji halisi tunao mbaroni na kuna kila ushahidi kuwa walimbambikia huyo mzee ili kujisafisha na tuhuma za mauaji ya huo binti…lakini sasa tuhuma zimewaganda. Niko tayari kuongea nawe juu ya ushahidi tulio nao dhidi yao…” Kwakwa alimwambia Inspekta yule mwenzake aliyekuwa katika kile kitengo cha “Albinism”. “Ah, Inspekta nadhani uko sahihi bwana..tuonane kesho tupeane dondoo ili nijithibitishie kuwa kweli mna ushahidi unaoonesha kuwa muuaji si huyu mzee. Kisha nitamwachia tu…” “Poa.” Zay alikuwa na furaha isiyo kifani alipopewa habari za kukamatwa kwa Chabi Cheka na Bilanga. “Ila nigekuwa na furaha zaidi iwapo wangekufilia mbali, wauaji wakubwa!” Alisema. “Ah, hili lililowakuta ni bora zaidi...wanaelekea kwenye hukumu ya kifo au kifungo cha maisha…na Chabbi ndio hatoweza tena kutembea, kutokana na tathmini ya awali ya madaktari…miguu imevunjwavunjwa vibaya sana kwa risasi...mwenywe anadai bora angeuawa tu!” Kwakwa alimwambia. “Sa si mngemuua tu? Mwenyewe kataka afe nyie mnabakisha bwana!” Zay alisema kwa hisia kali, na Pojo na Kwakwa wakatazamana. “Sheria haifanyi kazi hivyo bibie…” Kwakwa alimwambia. _________________ Asubuhi ya siku iliyofuata ilikuja na mshituko mkubwa kwa Zay, pale alipogongewa hodi na kuambiwa kuwa kuna mgeni wake. Alishangaa ni mgeni gani huyo lakini alipoona kuwa ni Boka mpenzi wake aliruka kwa furaha na kumkumbati kwa nguvu, furaha yake ikihamia kwenye kilio cha uchungu. “Okay, nice buttocks, the handsome guy is here to scare the ugly guys away, okay…? Relax babes!” Boka alimwambia kwa kubembeleza huku akiwa amemkumbatia kwa upendo, akimaanisha kuwa kijana mwenye mvuto, yaani yeye, ameshafika kuyafukuza majamaa yenye sura mbaya, na kwamba atulie tu. Hili liliamsha kicheko kilichochanganyika na kilio kutoka kwa Zay, na wote waili wakabaki wakiwa wamekumbatiana namna ile pale chumbani kwake kwenye kile kituo cha polisi kwa muda mrefu. “Inspekta Kwakwa amekuwa na msaada mkuwa sana kwangu, na amaeniambia kuwa sasa naweza kurudi nyumbani kwangu…maana wale watu wabaya tayari wameshakamatwa!” Zay alimwambia mpenziwe, na Boka akamuachia na kumkalisha kitandani. “Er, Zay…nilikuwa nimechukua jukumu bila kukushirikisha mpenzi, naomba usichukie…” Alisema na Zay akawa makini. “Ni nini tena mpenzi, mbona unanitisha?” “Si jambo baya sana…kama utalichukulia poa…” Boka alimjibu, na alipoona anazidi kumchanganya, akaendelea, “…nilikuwa nimechukua tiketi mbili za kurudi Rwanda babes...niliona baada ya maziko tungeenda wote kule, ubadili upepo kidogo.” Boka alimwambia huku akimtazama kwa mashaka. Zay alimtazama kwa muda kama kwamba alikuwa anamshangaa,kisha uso wake ukaachia tabasamu pana la furaha. “Aaa Dear, mbona ningependa sana iwe hivyooo!” “Ungependa?” Boka aliuliza huka akiwa amefarijika sana. “Of course dear, of course!” Zay alisema kwa furaha huku akijirusha tena kifuani kwa mpenziwe. Walikumbatiana kwa furaha. ________________ Maziko ya Mwamtumu yalifanyika saa saba mchana ule kule Gezaulole. Zay, Boka na wale maaskari wawili walihudhuria kule msibani, wale wanaume wakiienda hadi kule makaburini kuzika. Ilikuwa ni simanzi kubwa sana kwa Zay kujua kuwa rafiki yake ndio anaenda kwenye malalo ya milele. Muda wote alikuwa akifuatilia sana simu yake hasa kwenye mtandao wa facebook, na ilipotimu ile saa saba, muda ambao rafiki yake ndio alipangwa kulala kwenye malazi ya milele, kila kitu kikalipuka, na njozi za yule mwenyekiti wa kamati ya bunge ya maswala ya nishati kulizima sakata la kampuni ya Liquid Diamond zikayeyuka vibaya sana, tena kwa kishindo… Wakiwa kule makaburini, Inspekta Kwakwa alipigiwa simu na Mrakibu mwandamizi. “Kwakwa! Uko wapi wewe?” “Nilikwambia nitakuwa mazikoni kumzika Mwamtumu afande...vipi?” “Vipi? Kila kitu kimeharibika huku! Hakuna siri tena! Hivi nimeitwa kwa IGP huko, naye ameitwa kwa DCI..NI BALAA!” “Akh! Balaa la nini tena bosi? Bilanga katoroka?” “AKH! Ile ripoti ya Grayson…” “Imefanyaje?” “Iko wazi mtandaoni, watu… wananchi wamekuja juu vibaya sana mitandaoni humu…facebook inarindima Liquid Diamond tu.We ulitoa kopi ile ripoti kabla huajaiwasilisha kwangu?” Mrakibu alieleza na kuuliza. “Mimi? No! Sikuitoa kop...OH! Oh…!” Kwakwa alisema huku akili ikimjia juu ya kilichotokea. “Ni nini?” Mrakibu alimuuliza. Kwakwa alipiga kimya. “Nadhani najua ni nani aliyefanya hivyo afande!” Hatimaye alisema. “Ni nani huyo Kwakwa...ni nani?” “Ah! Nadhani ni Zay afande!” “Oh Shit!” Mrakibu alimaka na kukata simu. Kwakwa alimsaka Zay kule upande wa akina mama hadi akampata na kumwita pembeni, “Umefanya nini Zay…?” “Nimeizika Liquid Diamond Inspekta…muda ule ule ambao rafiki yangu anazikwa, na yenyewe inazikwa bloody fools. Nifanyeni lolote mtakalo!” Zay alimjibu na Kwakwa akabaki akimtazama kwa kutoamini. “Ni siku ile ulipoenda kuifuata hii ripoti kule kazini kwenu na ukatusubirisha nje kwa muda mrefu, sio? Ndio siku ulipohamisha ile ripoti kwenye mtandao wako?” Alimuuliza. “Nilijua ile ripoti ikifika kwa wakubwa zetu sitakuwa na mamlaka nayo tena. Na kweli! Nilitaka sana kuwalipua Liquid Diamond…na nimefanikiwa!” Zay alimjibu huku akimuonesha mtandao ule kupitia kwenye simu yake. Ukurasa wa facebook alioutengeneza na kuuita UFISADI WA LIQUID DIAMOND INCORPORATED ulikuwa umeanika wazi kila kilichotokea kwenye zile tafiti za nishati nchini, na jinsi mtafiti Grayson Mochiwa na rafiki yake Mwamtumu walivyouwa na watendaji wa ile kampuni iliyoaminiwa na serikali. Na mwisho ule ukurasa ukaianika wazi ile ripoti ya Grayson iliyofichwa, ikionesha jinsi utajiri wa gesi ulivyotanda kule Mtwara wakati wananchi wa huko wakiteseka kwa dhiki na umasikini. “Oh my God! Zay…! Umelipua bomu nchini…” Kwakwa alisema kwa mashaka. “Watu wanastahili kujua. Niliipanga hii habari itoke hewani ikifika saa saba kamili mchana leo hii...na naona nimefanikiwa!” Zay alisema kwa ushindi. Asubuhi iliyofuata Zay alipaa na Boka kuelekea Rwanda. _______________ Kufuatia habari ile kuruka hewani, waziri wa madini na nishati aliagiza Mkurugenzi wa makosa ya jinai nchini afanye uchunguzi wa kina, na kwa kuwa watuhumiwa wote muhimu walikuwa mbaroni haikuchukua muda kabla mwenyekiti wa ile kamati ya bunge hajang’amuliwa na kamati yake kuvunjwa. Hatua nyingine za kisheria ziliendelea kuendeshwa dhidi yake. Kambesera, Bilanga na Chabbi Cheka walifungwa vifungo vya maisha kwa makosa ya kuhujumu nchi na pia kupanga njama na kutekeleza mauaji ya Grayson Mochiwa na Mwamtumu. Boka alisaini mkataba mrefu zaidi kule Rwanda, na akafanikiwa kumpatia Zay kazi kwenye kasini kubwa sana jijini Kigali, ili tu awe naye kule nchi ngeni. Mijadala yao ikawa inaelemea zaidi kwenye ndoa wakiwa huko… Kutokana na habari ya gesi ya Mtwara kuwekwa wazi na Zay kupitia mtandao na kupambishwa vilivyo na vyombi vya habari, wanachi wa Mtwara nao wakaja juu, wakiidai gesi yao kwa nguvu moja. Kwa miezi kadhaa, nchi iliingia kwenye mtafaruku wa gesi ya Mtwara, na kwa namna fulani swala la Zay kurusha ile habari hewani likapotea tu, na ule ukurasa wake wa facebook ulioianika Liquid Diamond ukafutwa. Inspekta Kwakwa alihamishiwa moja kwa moj akwenye kitengo cha majukumu maalum chini ya bosi wake wa zamani John Vata, na Sajendi Pojo alipandiswa cheo na kuhamishiwa polisi makao makuu. MWISHO ***Nawashukuru sana kwa kuwa nami kwa takriban mwezi mmoja na nusu tukishirikiana kukiendesha kisa hiki. Binafsi nimefarijika sana kuwa nanyi hapa konani. Natumai mtaendelea kuwa nasi hapa konani ili tuendeleze tasnia hii ya uandishi na usomaji. Wengi mmeomba kitabu cha kisa hiki, nami nawaahidi kuwa kitabu mtakipata…kikiwa na mengi kuliko haya mliyoyasoma hapa. Ahsanteni, Hussein Tuwa.
Posted on: Tue, 15 Oct 2013 14:59:50 +0000

Trending TopicsRecently Viewed Topics
© 2015