Rebecca (52) Ilipoishia jana... Baada ya muda majirani - TopicsExpress



          

Rebecca (52) Ilipoishia jana... Baada ya muda majirani wakakusanyika kwa mzee Kimaro na walipoiona hali ile walipiga simu polisi. Walipofika walizitoa maiti za James na mlinzi wakaziingiza garini kisha Rebecca aliyekuwa mahututi alipakiwa kwenye tori tori na kukimbizwa hospitali. Saa 8:20 usiku Rebecca aliingizwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali. Mzee Kimaro akaingizwa chumba kingine na kupatiwa matibabu kwenye bega lake ambako alifungwa bendeji ngumu. Endelea... Asubuhi hii, John alichelewa kuamka tofauti na siku nyingine hasa siku kama ya leo yaani jumatatu. Alikuwa anaamka saa kumi na moja alfajiri akaenda mazoezini. Jumatatu hii aliamka saa moja unusu. Kwa muda huu hakuweza kwenda mazoezini, bali alifanya mazoezi chumbani kwake. Alipiga push up kwa muda wa nusu saa. Alipomaliza alijifunga taulo kiunoni, akabana mswaki kinywani na ndoo ya maji mkononi. Akaingia bafuni. Aliporudi huko, akajiandaa vizuri na kutoka nje. Akaenda moja kwa moja hadi sebuleni, akamkuta mzee Matamahuluku anakunywa chai. “Mi nimekusubiri hadi nikashindwa, nimeamua kutangulia.” “Haina shida mzee, najua huwezi kumaliza.” “Usifanye masihara kijana, hii ni mashine kubwa. Udongo wa zamani huu.” “Hahahahaa! Kama udongo wa zamani unadhani utashindana na udongo huu wa sasa. Hebu tushindane basi. Umekula vitumbua vingapi, nikulipe?” “Hahahahaha!” “Shikamo.” “Marhaba, vipi hujambo?” “Sijambo, mwenyewe si unaniona?” “Mbona hukwenda mazoezini?” “Nimechelewa kuamka. Ila nimefanya ghetto.” Wakaongea huku wanafungua kinywa. Na baada ya kumaliza kufungua kinywa, John aliaga na kuondoka. “Wapi leo baba?” “Nafika hapo kwa rafiki yangu mmoja hivi.” “Haya tutaonana baadaye.” Akiwa anatoka pale sebuleni kutoka nje, aliingiza mkono mfukoni na kutoa simu, ilikuwa bado imezimwa tangu jana alipopigiwa simu na mtu asiyemfahamu ambapo hakupokea ila aliizima. Sasa alitaka kuiwasha ili awasiliane na rafiki yake aliyepanga waonane asubuhi hii. Akaiwasha. Sekunde chache baada ya kuiwasha, ikaingia sms, namba ngeni. Akaiangalia kwa makini na kubaini ni ile iliyompigia jana mchana na kuzima simu badala ya kupokea. “Unavyofanya siyo vizuri, unapigiwa simu hupokei na unazima. Ukitumiwa sms hujibu. Nakuomba umtafute Rebecca haraka iwezekanavyo kwa usalama wako. Ukipuuza utalia peke yako… Isabela.” Ujmbe huu ulitumwa jana majira ya saa mbili usiku. Kutokana na John kuzima simu,unaingia leo baada ya kuiwasha. “Isabela! Ni nani huyu?” John akajiuliza, lakini baada ya kurudisha kumbukumbu, alimkumbuka. “Anha, ni yule mhudumu wa mapokezi waliyekuja na askari pale hotelini. Ameipataje namba yangu na ana maana gani kusema nimtafute Rebecca haraka iwezekanavyo.” Punde tu alipomaliza kuusoma ujumbe wa Isabela, ukaingia ujumbe mwingine, nao ulitumwa na namba ngeni, “Bwana John vipi mbona kimya sana, kulikoni? Naomba umtafute Rebecca au tutafutane, ni muhimu sana.” Tofauti na ujumbe wa kwanza huu haukuwa na jina la mtumaji. Pia ulionesha umetumwa jana usiku. “Kuna nini, mbona kila ujumbe una agizo linalofanana? Na huyu naye, ni nani. Ana nini Rebecca.” Hakupata majibu na majibu wanayo hawa waliomtumia ujumbe, Isabela na huyu asiyeandika jina lake. Kabla hajajua afanye nini, simu yake ikaita, alipoiangalia namba ya mpigaji, akagundua ni ile iliyomtumia ujumbe muda mfupi uliopita. Kwanza hakutaka kupokea, alipokumbuka sms zilizoingia muda mfupi na msisitizo uliomo hasa hii ya pili, akaamua kupokea. “Hallo!” “Hallo John, dereva wa Rebecca hapa nina shida na wewe. Uko wapi?” “Mi niko mitaa ya home huku, ila nilikuwa natoka, kuna nini?” “Niambie uko wapi nikufuate. Ni muhimu sana.” “Basi naomba nikukute hapo mission.” “Fanya haraka.” Dakika chache John alikuwa pale mission na kumkuta dereva akimsubiri. Alipomuona John, dereva alimfungulia mlango na kumuashiria aingie garini. Alipohakikisha John ameingia na kukaa vizuri, dereva aliwasha gari na kuondoka. “Vipi John mbona kimya kimekuwa kingi sana?” “Mambo tu mzee wangu.” Waliongea maneno machache, kisha kimya huku dereva anakanyaga mafuta. *************** Tangu ameingizwa chumba hiki cha wagonjwa mahututi usiku wa manane, Rebecca hakuwa katika hali ya kawaida. Alionekana kama hana muda mrefu ataaga dunia. Hii ni kutokana na kupoteza damu nyingi katika majeraha na kucheleweshwa kupata huduma ya kwanza. Madaktari walifanya juhudi kubwa kuhakikisha wanayaokoa maisha yake. walimfanyia upasuaji kifuani na kutoa risasi. Jambo la kushukuru ni kwamba hakuathirika sana na risasi ila kilichomfanya awe hivi ni kupoteza damu nyingi na lile jeraha la kichwani ambalo lilitokana na kujipiga kwenye televisheni. Lilimpasua fuu kule kisogoni, pia kutokana na kujipiga huko, ubongo wake ulicheza na kiasi fulani cha damu kilivujia kwa ndani. Ingawa alikuwa anapumua wakati anaingizwa chumbani humu, alipumua kwa shida na hakujitambua. Walipomshughulikia, kidogo alipata nafuu, hivyo walimtoa katika chumba cha wagonjwa mahututi na kumpeleka katika wodi ya kulipia. Kwa msaada huu wa madaktari, walifanikiwa kumzindua, japo bado alipumua kwa shida. Neno ambalo lilikuwa kinywani mwake kila alipozinduka, lilikuwa ni John. Atalala, lakini akishtuka tu, John. Hali hii ikamfanya daktari mkuu aliyesimamia shughuli zote za matibabu, kuulizia huyu John ni nani. Akajibiwa na mama yake kuwa ni mtu aliyefikiria kuishi naye maishani. Kwa hivi daktari akashauri basi huenda ahueni zaidi itapatikana endapo huyo mtu ataletwa na amuone. Ilikuwa ngumu sana namna ya kumpata hadi pale alipofika dereva pale hospitali baada ya kupata taarifa usiku. Wakamuuliza kama anamjua huyo John na anakoishi. Dereva akawaambia alishawahi kumuona mara kadhaa hasa kipindi wanasoma tuition na hata majuzi tu alimuona. Pia jana usiku alipewa kazi ya kumtafuta na alimtumia sms lakini ilikuwa bado haijapokelewa baada ya kumpigia simu na kuonesha haikuwa hewani. Akaambiwa amtafute haraka sana. Wakiwa wanaendelea kujadiliana namna ya kumpata, simu ya dereva ikaingia sms, alipoangalia, akaona ni taarifa ya kupokelewa sms aliyoituma jana usiku. Hii iliashiria kuwa simu ya John iliwashwa. Ndipo akampigia na kuongea naye. ************** Itaendelea kesho!. Tunawatakia siku njema___
Posted on: Tue, 29 Oct 2013 02:13:08 +0000

Trending Topics



Recently Viewed Topics




© 2015